Kuswali mabega wazi (Singlend)
Question
Je, inajuzu kisharia kwa mtu kuswali akiwa mabega yake yako wazi — yaani amevaa kile kinachoitwa "Singlend?
Answer
Wanazuoni wa Fiqhi wamekubaliana (wanachuoni wa Sharia) ni wajibu kusitiri uchi katika Swala. Kwa mwanamke, uchi wake ni mwili mzima isipokuwa uso na viganja vya mikono. Kwa mwanamume, uchi wake ni kuanzia kitovuni hadi magotini.
Hata hivyo, inajuzu kwa mwanamume kuswali akiwa amevaa fulana isio na mikono kwa mujibu wa Wanachuoni wote wa Fiqhi, hata wale waliowajibisha kusitiri mabega; kwa sababu kusitiri mabega kunapatikana hata kwa kamba nyembamba. Lakini, inapendekezwa kisharia kwa Muislamu kuvaa nguo nzuri na bora zaidi alizonazo wakati wa Swala, kwani anakuwa katika hali ya kuelekea mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu
Maelezo
Ni amri ya kisharia kuwajibika kusitiri uchi wakati wa Swala; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: "Enyi wana wa Adam! Chukueni mapambo yenu (nguo zenu) katika kila mahali pa ibada (msikiti)" [Al-A'raf: 31]. Makusudio ya "mapambo" katika Aya hii - kama walivyosema Wanachuoni - ni nguo zinazositiri uchi; kwani Aya hii ilishuka kwa ajili ya washirikina waliokuwa wakitufu Al-Kaaba wakiwa uchi., kusitiri uchi ni jambo ambalo halina tofauti miongoni mwa Wanachuoni [[1]].
Pia, inapendekezwa kisharia kwa mwanadamu kuvaa nguo bora zaidi katika Swala yake, na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu kwa nguo nzuri kabisa anazoweza kupata [[2]].
Aina za uchi zinazopaswa kusitiriwa katika Swala ni mbili:
Aina ya Kwanza: Uchi wa mwanamke katika Swala yake: Imeamuliwa kisheria wajibu wa mwanamke kufunika mwili wake katika sala isipokuwa uso na vigaanja vya mikono. Kutoka kwa Aisha (R.A), kutoka kwa Mtume S.A.W. amesema: "Mwenyezi Mungu hakubali Swala ya mwanamke aliyebaleghe isipokuwa akiwa na ushungi (khimar [3])" [Imepokelewa na Abu Dawood].
Kutoka kwa Umar bin Al-Khattab (R.A) amesema: "Mwanamke aswali katika nguo tatu: Gauni, sketi na ushungu .". Hadithi hizi za Mtume zinafahamisha kuwa ni wajibu kwa mwanamke kusitiri mwili wake wote katika Swala isipokuwa uso na vitanga vya mikono.
Aina ya pili: Uchi wa mwanamume katika Swala yake:
Ni makubaliano ya Wanachuoni kuwa uchi wa mwanamume ni kuanzia kitovuni hadi magotini, na ndiyo sehemu inayopaswa kusitiriwa ndani na nje ya Swala. Kutoka kwa Abdullah bin Jafar bin Abi Talib amesema: Nilimsikia Mtume (S.A.W). akisema: (Kati ya kitovu na goti ni uchi) Imepokelewa na An-Nasaai.
Kuhusu mwanamume kuswali akiwa mabega yake yako wazi -yaani amevaa kile kinachoitwa "Singlend” - wanachuoni wametofautiana kama ifuatavyo:
Rai ya Kwanza ni rai ya Hanbali: Kwamba ni miongoni mwa masharti ya kusihi kwa Swala kwa mwanamume kusitiri mabega wakati wa Swala, iwe Swala ya faradhi au Sunna. Hoja yao ni Hadithi ya Abu Hurairah (R.A). kwamba Mtume (S.A.W). amesema: "Asiswali mmoja wenu katika nguo moja ikiwa hakuna chochote katika bega lake. Imepokelewa na Annasaaiy. " Wamesema makusudio ya Hadithi ni uwajibu wa kusitiri mabega.
Maoni ya pili (Wengi miongoni mwa Wanachuoni wa Fiqhi): Kwamba inajuzu kwa mwanamume kuswali mabega yakiwa wazi, na hakuna kosa mradi tu alichovaa kimesitiri uchi (kati ya kitovu na goti). Mabega si sehemu ya uchi kwa mwanamume. Kuhusu Hadithi ya Abu Hurairah, wamesema kuwa inamaanisha kupendeza (Mustahabb) mwanamume kusitiri mabega kwa chochote hata kama ni uzi mwembamba; kwani kuswali kwa nguo inayofunika nusu ya chini tu bila ya juu ni jambo linalochukiza kidogo (Makruh Tanzihi) lakini si haramu [[3]].
Rai yenye nguvu ambayo ndiyo inayotolewa Fatwa na Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri ( Dar Al-Ifta ya Misri) ni maoni ya pili yanayosema: Inajuzu mwanamume kuswali akiwa mabega yake yako wazi (amevaa fulana ya kamba), kwa sababu zifuatazo:
Kwanza: Amri ya kusitiri mabega katika Hadithi ya Abu Hurairah inatafsiriwa kama mapendekezo (Sunna) na si uwajibu.
Pili: Mwanamume anayesawli akiwa amevaa "Singlend" anakuwa amekidhi pia vigezo vya wale waliowajibisha kufunika mabega; kwani kusitiri bega hata kwa kamba nyembamba kunahesabika kama ni kuyafunika [[4]]. Kwa namna hiyo, anakuwa ametoka katika hitilafu za Wanachuoni.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Jambo walilokubaliana Wanachuoni wa Fiqhi ni wajibu wa kusitiri uchi wakati wa Swala. Kwa upande wa mwanamke, uchi wake ni mwili mzima isipokuwa uso na viganja vya mikono. Kwa upande wa mwanamume, uchi wake ni sehemu iliyopo kati ya kitovu na magoti.
Inajuzu kwa mwanamume kuswali akiwa amevaa kile kinachoitwa "Singelnd" kwa mujibu wa Wanachuoni wote wa Fiqhi, hata kwa wale waliowajibisha kusitiri mabega; kwa sababu kusitiri mabega kunapatikana hata kwa kuwepo kwa kamba au uzi mwembamba.
Inapendekezwa kisharia (Mustahabb) kwa Muislamu kuvaa nguo nzuri na bora zaidi alizonazo wakati wa Swala; kwa sababu anakuwa katika hali ya kuelekea na kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
[1] Al-Tamhid cha Ibn Abdil-Barr (6/376).
[2] Bada'i al-Sana'i cha Al-Kasani (1/219).
[3] Al-Majmu' cha An-Nawawi (3/175).
[4] Kifayat al-Nabih cha Ibn al-Rif'ah (2/470).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
