Kukusanya Swala bila udhuru
Question
Je, inajuzu kukusanya Swala mbili (kama Adhuhuri na Alasiri, au Magharibi na Isha) bila ya kuwa na udhuru wa kisharia?
Answer
Kutekeleza Swala za faradhi katika wakati wake ni jambo linalopendekezwa kisharia (mustahabb), na ni miongoni mwa matendo yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu. Kukusanya sala kwa sababu ya udhuru kama vile ugonjwa, safari, na mambo kama hayo, ni jambo linalokubalika kisharia kwa mujibu wa makubaliano ya wanachuoni wengi (Jamhur al-Ulama).
Hata hivyo, kukusanya Swala za faradhi bila ya udhuru—kwa ajili ya kukidhi haja fulani ya dharura au kushughulika na kazi na mfano wake—ni jambo linalojuzu kisharia kwa sharti kwamba lisifanywe kuwa ni mazoea ya kila siku. Haifai kumkemea au kumlaumu anayekusanya sala bila udhuru (katika hali ya dharura ya mara moja), kwa sababu jambo hilo limethibiti katika Hadithi za Mtume (S.A.W). kama njia ya kuwafanyia watu wepesi na kuondosha uzito.
Maelezo
Imethibiti kisharia kuwa Sala ni nguzo ya Uislamu na ni nguzo ya pili baada ya Shahada mbili. Mwenyezi Mungu Anasema: " Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanao inama..." [Al-Baqarah: 43], na anasema: "Hakika Sala kwa waumini ni fadhila iliyowekewa nyakati maalumu" [An-Nisa: 103]. Kutoka kwa Abdullah bin Umar (R.A). amesema: Mtume (S.A.W). amesema: (Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: Kushuhudia kwamba hapana mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kusimamisha Sala, na kutoa Zaka, na kwenda Hija, na kufunga mwezi wa Ramadhani) Imepokelewa na Bukhari.
Ni jambo linalopendekezwa kwa Muislamu kuharakisha kusali mapema wakati unapoingia. Katika hadithi ya Ibn Mas'ud, Mtume (S.A.W). aliulizwa ni tendo gani linalopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu, akajibu: "Sala katika wakati wake." Nikasema: Kisha nini? Akasema: Kisha kuwafanyia wema wazazi wawili (Birrul-Walidayn). Nikasema: Kisha nini? Akasema: Kisha kupigana Jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu) Imepokelewa na Bukhari.
Faida ya Hadithi hii ni kwamba kutekeleza Swala katika wakati wake wa kwanza ni miongoni mwa matendo bora na yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu S.W.T.
Uislamu umeipa Swala umuhimu mkubwa sana, kiasi kwamba umewaamrisha Waislamu kuilinda (kuitekeleza) kwa umakini wakiwa nyumbani (wakati wa makazi) au safarini, wakati wa amani au wa hofu, na wakati wa utulivu au wa vita. Hata katika mazingira magumu zaidi, wakati hofu inapozidi pale Waislamu wanapokuwa katika uwanja wa vita mbele ya adui, bado amri ya Swala inabaki.
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Anasema:"Zichungeni Swala, na hasa Swala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kunyenyekea. Na ikiwa mna hofu, basi salini mkitembea kwa miguu au mkiwa mmepanda (wanyama/vyombo vya usafiri). Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafundisha yale mliyokuwa hamyajui." [Al-Baqarah: 238-239]. Maana yake ni: Swalini mkiwa katika hali ya hofu na vita, mkiwa mnatembea kwa miguu au mmepanda (wanyama/vyombo) kwa namna yoyote mnavyoweza, bila ulazima wa rukuu wala sijida kamili, bali kwa kuashiria tu (kwa kichwa au macho), na bila sharti la kuelekea Qibla ikiwa hali hairuhusu. Mwenyezi Mungu anasema: "Na Mashariki na Magharibi ni za Mwenyezi Mungu; basi kote mnapogeukia, huko kuna uso wa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenezi (na) Mwenye kujua." [Al-Baqarah: 115].
Sheria ya Kiislamu imeruhusu kukusanya sala (Jam'u) kwa ajili ya udhuru (sababu maalumu), kama vile: Anapokuwa katika huduma ya kijeshi kukusanya sala kwa sababu ya hofu ya adui, au kwa ajili ya kulinda doria katika eneo analolilinda kwa ajili ya kuitetea nchi, au dkatari Kukusanya Swala kwa sababu ya kushindwa kutoka katika chumba cha upasuaji (theatre), au kwa sababu ya safari au sababu kama hizo.
Namna ya kukusanya Swala (Jinsi ya Kuswali):
Kukusanya Swala kunafanyika kwa namna ifuatayo:
Kukusanya Swala ya Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja wakati wa Adhuhuri (Jam'u Taqdim).
Kukusanya Swala ya Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja wakati wa Alasiri (Jam'u Ta-khir).
Kukusanya Swala ya Magharibi na Isha kwa pamoja wakati wa Magharibi (Jam'u Taqdim).
Kukusanya Swala ya Magharibi na Isha kwa pamoja wakati wa Isha (Jam'u Ta-khir).
Ama Sala ya Alfajiri, wakati wake unaanza tangu kuchomoza kwa alfajiri (na haikusanywi na sala nyingine).
Dalili ya Jambo Hili:
Ni Hadithi iliyopokelewa na Mu'adh bin Jabal (R.A) amesema: (Tulitoka pamoja na Mtume (S.A.W). katika vita vya Tabuk, akawa anasali Adhuhuri na Alasiri pamoja, na Magharibi na Isha pamoja) imepokelewa na Muslim.
Ama kuhusu suala la kukusanya Swala bila ya udhuru wa kisharia (kama vile safari au ugonjwa), kwa mfano kwa ajili ya kukidhi haja fulani au mtu kushughulika na kazi na mambo kama hayo, Wanachuoni wa Fiqih wametofautiana katika hukumu hiyo katika rai mbili:
Kwanza: Haijuzu kisharia kukusanya Swala bila ya udhuru. Msingi ni kwamba Swala za faradhi lazima zitekelezwe katika wakati wake maalumu, na kukusanya Swala ni lazima kuwe na sababu maalumu kama alivyofanya Mtume (S.A.W.) katika vita vya Tabuk.
Pili: Inajuzu kisharia kukusanya Swala bila ya udhuru (kwa ajili ya kukidhi haja maalumu au kushughulika na kazi na mfano wake), kwa sharti kwamba jambo hilo lisiwe ni tabia au mazoea ya kila siku ya mtu [[1]].
Rai yenye nguvu ambayo imechukuliwa na Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri (Dar Al-Ifta ya Misri) , ni rai ya pili ianayosema: Inajuzu kisharia kukusanya Swala bila ya udhuru wa kawaida, kwa ajili ya haja maalumu au kushughulika na kazi na mfano wake, lakini kwa masharti yafuatayo:
Kwanza: Mtu asichukue ukusanyaji wa Swala kuwa ni tabia au mazoea ya kila siku.
Pili: Mtu aweke nia ya kukusanya Swala wakati anapotekeleza Swala hizo.
Tatu: Pasiwe na muda mrefu wa kupita kati ya sala hizo mbili, bali uwe muda mfupi tu, na kipimo cha muda huo kinategemea mazoea na desturi ya watu (Al-Urf) [[2]].
Sababu za kuona sahihi rai ya kukusanya Swala bil ya dharura ni kama ifuatavvyo:
Kwanza: Sharia ya Kiislamu imejengwa juu ya wepesi na kuondoa uzito kwa walikalifishwa. Mwenyezi Mungu Anasema: "...Mwenyezi Mungu Anakutakieni wepesi na wala hakutakieni uzito..." [Al-Baqarah: 185]. Na amesema Mtukufu: "Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni (uzito), na mwanadamu ameumbwa akiwa dhaifu" [An-Nisaa: 28]. Imepokewa Kutoka kwa Abi Umama (R.A) Mtume (S.A.W). amesema: "Nimetumwa na dini ya kweli (Al-Hanifiyyah) iliyo nyepesi" [[3]].
Kukusanya Swala kunaleta wepesi kwa watu katika kutekeleza Swala za faradhi wanaposhughulika nazo nyakati fulani kwa ajili ya kukidhi haja au kumaliza baadhi ya kazi na mfano wake.
Pili: Imekuja katika Hadithi za Mtume (S.A.W) kuna ushahidi wa kujuzu kukusanya Swala bila udhuru; ikiwa ni kwa ajili ya kuwapunguzia na kuwaondolea uzito watu; Kutoka kwa Abdullah bin Abbas (R.A). amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W). alikusanya Adhuhuri na Alasiri, na Magharibi na Isha mjini Madina, bila ya kuwepo hofu wala mvua". Alipoulizwa Ibn Abbas: "Kwa nini alifanya hivyo?" Akasema: "Ili asiiletee uzito kwa umma wake". Na katika mapokezi mengine: "Alitaka asiuingize umma wake katika uzito"(Imepokelewa na Muslim).
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Kutekeleza Swala za faradhi katika wakati wake maalumu ni jambo linalopendekezwa kisharia (Mustahabb), na ni miongoni mwa matendo yanayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kukusanya Swala za faradhi kwa ajili ya udhuru kama vile ugonjwa, safari, na mambo kama hayo, ni jambo linalojuzu kisharia kwa makubaliano ya wanachuoni wengi.
Kukusanya Swala za faradhi bila ya udhuru wa kawaida, kwa ajili ya kukidhi haja fulani au mtu kushughulika na kazi na mfano wake, ni jambo linalojuzu kisharia kwa sharti kwamba jambo hilo lisiwe ni tabia au mazoea ya kila siku ya mtu.
Haifai kumkemea au kumlaumu yule anayekusanya sala bila udhuru (kwa ajili ya haja maalumu); kwa sababu jambo hilo limethibiti katika Hadithi za Mtume (S.A.W). kama njia ya kuwapunguzia watu uzito na kuwafanyia wepesi.
[1] Angalia: «Al-Majmu'» cha An-Nawawi (4/384), «Rawdat al-Talibin» cha An-Nawawi (12/401), «Al-Mughni» cha Ibn Qudamah (2/205), na «Fath al-Bari» cha Ibn Hajar (2/24).
[2] Hashiyat al-Adawi 'ala Sharh Kifayat al-Talib al-Rabbani (1/336).
[3] Imepokelewa na Ahmad katika Musnad yake (36/624).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
