Kunyanyasa watoto na mke.
Question
Mume wangu alijaribu kunikinaisha kuwa pigo la mume kwa mkewe na kumuadabisha na kumtisha na kumtia hofu pia kwa watoto ni katika mambo yanayofaa kwa mujibu wa sharia ya kiislamu. Pamoja na kuwa ninasoma Qur`ani Tukufu siku zote ila nimehisi kuwa jambo hili si sahihi bali niliona kinyume chake kuwa Uislamu ni dini ya huruma na upole.
Je, madai ya mume wangu ni sahihi?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Uislamu ni dini ya huruma, na Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume wake (Rehma na amani zimshukie) kuwa ni rehema kwa walimwengu, akasema {Nasi Hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu} (AL ANBIYAA 107). Na sharia ikasisitiza haki ya mtu dhaifu kwa kuonewa huruma, na mmoja wa hao (madhaifu) ni mwanamke. Mtume (Rehma na amani zimshukie) akaseama: “Ewe mola wangu mimi ninapata tabu kwa haki ya hawa madhaifu wawili: Yatima na mwanamke”. Imepokewa na An nasaai na Ibn Majah kwa mapokezi ya hukumu ya Hadithi Hasan, na kama alivyosema Imamu Annawawiy katika kitabu cha: [Riyadh Aswalihina].
Na mwanamke ana haki ya kuonewa huruma kuliko mwingine kutokana na udhaifu wa mwili wake na kuhitaji kwake atakayemsaidia mambo yake kwa muda mrefu. Ndio maana Mtume (Rehma na amani zimshukie) akawafananisha wanawake na kioo kutokana na wepesi na ulaini pamoja na udhaifu wa miili yao, akasema kumwambia Anjashah: “Ole wako ewe Anjashah, kuwa makini na vioo”. Imepokewa na Muslim na Bukhari.
Na wasomi wa kiisilamu wakaifahamu kauli hiyo na kuifanyia kazi inavyopasa mpaka ikawa miongoni mwa taabia zao ambazo zimetengeneza misingi ya fikira zao za Kifiqhi: “Uke ni udhaifu wa kudumu wenye kustahiki kuchungwa siku zote”.
Na Uislamu umemtaka mume awe mwema katika kuishi na mkewe, na Mwenyezi Mungu amesema kuwa maisha ya ndoa yamejengeka kwa misingi ya utulivu, upendo na huruma akasema {Na katika Ishara Zake ni kuwa Amewaumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao, naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika hayo zimo Ishara kwa watu wanaofikiri} (AR RUUM 21)
Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) amefanya kigezo kizuri katika maisha ya ndoa kwa waume kuwafanyia wema wake zao, akasema: “Mbora wenu ni aliye mbora kwa watu wake (wake zake), nami ni mbora kwa watu wangu”. Amepokea At Tirmidhi kutoka kwa Aisha (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie).
Na sharia ikasisitiza upole katika kutatua makosa, na Mtume akahimiza upole pia litokezeapo jambo kama hilo, akasema: “Hakika ya upole hauwi kwenye kitu isipokuwa hukipamba, na wala hauondoshwi kwenye kitu isipokuwa hukiharibu”. Imepokewa na Muslim kutoka katika Hadithi ya mama wa waumini bibi Aisha (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie).
Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) hakuwahi kuwapiga hata mara moja wake zake, imepokewa kutoka kwa mama wa waumini bibi Aisha (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) amesema: “Mtume (Rehma na amani zimshukie) hakukipiga kitu kwa mkono wake hata mara moja, wala (hakumpiga) mwanamke wala mtumishi isipokuwa anapokuwa katika jihadi kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, na hakupata kitu (kitu cha mtu mwengine) chochote akawa anataka kumwangamiza mwenye kitu hicho isipokuwa atakapokuwa (mutu huyo) anataka kuvunja mipaka ya Mwenyezi Mungu hapo hukiangamiza kitu hicho”. Imetolewa na Muslim.
Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) ni mfano mwema ambao ni lazima kwa wanandoa wamfuate kwa njia zake njema katika kuamiliana na wake zao, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu {Bila shaka mnao mfano mwema katika Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana} (AL AHZAAB 21).
Na imepokewa ndani ya Qur`ani kuhusu kupigwa kwa mke katika sehemu moja kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na (wanawake) ambao mnaogopa uasi wao, basi waonyeni na waacheni peke yao katika vitanda, na wapigeni. Na kama wanawatii, basi msiwatafutie njia. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye juu, Mkuu.} (AN NISAA 34).
Na uasi, ni kule kwenda kinyume na maadili na jamii na ikawa mwanamke anajizuia kutimiza wajibu wake na wajibu huo ni haki za mume na kama ilivyokuwa haki za mume huzingatiwa kuwa ni miongoni mwa wajibu upasao kutekelezwa na mke, kwa kwenda kinyume na hivyo huwa amekwenda kinyume na jamii na maadili ambayo Mwenyezi Mungu amemwongoa mwanamme kwa ajili ya kutaka kuongoka kwa wake zao, nayo ni kwa mujibu wa mazingira ya kila mke kwa upande, na kwa mujibu wa ada iliyoenea katika utamaduni na mazingira ambayo mke amekulia ambayo mara nyingi humili katika kuleta masilahi ya mwanamke, na mpangilio huu wa (kuanza na mawaidha na kuja tendo la kupiga) ni lazima ufuatwe kwa dalili ambayo ni kule kuwepo kwa kiunganishi cha “na” na si kiunganishi cha “kisha” hivyo mume ataamali na mkewe kwanza kwa kumuonya (kumpa mawaidha) nayo ni kwa maneno mepesi na kumkubusha kuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu na haki zake (haki za mume) ambazo anahitajika kuzitimiza. Na kama sheria ilivyoruhusu kumhama kitandani katika kufanya jaribio la kumshinikiza ili aweze (mke) kutekeleza wajibu wake pasi na kumdhulumu au kumfanyia uadui, na masharti yake ni kuwa yasivuke mipaka ya kumdhuru mwanamke kinafsi.
Ama chaguo la kumpiga lililotajwa katika Aya: Wanazuoni wamekubaliana kwa tamko moja kuwa haikusudiwi kumpa mke maumivu au kumdhalilisha, isipokuwa Aya imekuja kuhalalisha baadhi ya hali ambazo haitakuwa ni lazima (hali) hizo kuwa ndiyo zitekelezwe, na kwa baadhi ya mazingira (mengine) ambayo matendo kama haya huwa hayazingatiwi kuwa ni udhalilishaji wa mke wala kumbughudhi, kwa kuwa mume itaonekana kuwa anaonesha kuwa kachukizwa na anasisitiza kuwa amekerwa na jambo fulani la wajibu, hapo atampiga pigo dogo (lisiloumiza) na lisiloacha athari akikusudia kumkanya na kumkemea, nalo litakuwa kwa mswaki na mfano wake katika zana ambazo kwa kawaida huwa hazitumiwi kama kitu cha kupigia.
Hadithi imetolewa na Ibn Jarih kutoka kwa Atwaa amesema: nilimwambia Ibn Abas (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie): “Ni pigo gani lisiloumiza? Akasema: “Pigo la mswaki na mfano wake”.
Na kuna tafauti kubwa ya pigo la mswaki ambalo halikusudiwi kuumiza na baina ya utumiaji wa nguvu au bakora au kuumiza au kudhalilisha. Na Wanazuoni wameelezea kuhusu pigo hili jepesi (lisiloumiza), iwe ndio hali ya mwisho ambayo mume ataitumia, na wala haitafaa kumhama (mke) na kumpiga kwa sababu tu ameasi kabla ya kutafuta suluhisho.
Na pigo hili lisiloumiza (jepesi) litakuwa ni haramu iwapo mume atajua kuwa suluhu inaweza kupatikana bila ya kutumia njia hii, vilevile wameelezea uharamu wake iwapo mume atajua kuwa hata akimpiga suluhu haitapatikana au anaweza kumjeruhi au kumuacha na athari.
Imamu Al hatwab Al maliki anasema katika kitabu cha: [Mawahib Al jalil 15-16]: “Iwapo dhana yake itakuwa na uhakika kuwa pigo halitasaidia, basi hatahitajika kumpiga. Mwisho wa kunukuu.
Na katika kitabu cha: [Al Jawahir] “Iwapo dhana yake ina uhakika kuwa mke hataacha uasi isipokuwa kwa kupigwa sana basi haitapasa (kupigwa) wala kupewa adabu. Mwisho wa kunukuu. Na pia imenukuliwa kutoka kwa Ibn Arafa.” Mwisho.
Pia Maulamaa wamenukuliwa kusema kuwa hata mume naye hupigwa na kupewa adabu akikosea katika haki za mke kwa mfano akiitoa bikira ya mkewe kwa kidole chake. Imam Dardir amesema katika kitabu cha: [Ash Sharhu Swaghir Hashiya As Shykh Swawiy 4/392, chapa, Dar Al Maarif]: “Kuondoa bikira kwa kidole ni haramu, na mume atapewa adhabu juu ya hilo.” Mwisho.
Na Wanazuoni wametilia mkazo juu ya maana hii, wapo walioeleza kuwa haipasi kumpiga mke kwa bakora au fimbo na mfano wake, lakini iwe kwa mkono au mswaki hii ni kwa kuonesha kuwa amechukia tu.
Kama ilivyoeleza Hadithi ya Ibn Abbas (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie) ilivyotangulia. Na amaepokea Ibn Abi Hatim katika tafsiri yake kutoka kwa Al hasan Al baswari kuwa yeye ameifasiri pigo jepesi (lisiloumiza) ni lile lisilokuwa (lisiloacha) athari (alama za mapigo). Na haitafaa kukusudia kumuumiza lakini iwe kwa nia ya kumuadabisha (tu), na wameelezea kuwa ni lazima aepukane na maeneo yanye kupelekea mauaji na ajiepushe na sehemu nyeti ambazo zinahisiwa kuwa kumpiga katika sehemu hizo ni kumdhalilisha, kwa mfano; usoni, kichwani, shingoni, kwenye tupu na kisogoni, kama alivyosema Mtume (Rehma na amani zimshukie) “mmoja wenu akipigana basi ajiepushe na uso” Bukhari na Muslim kutoka kwa Hadithi Abi Hurayra (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie). Na wala haifai pigo liwe kubwa wala la kutoa damu (kujeruhi) wala la kuumiza kwa namna yeyote ile.
Hivyo, pigo lililotajwa katika aya ya Qu`rani Tukufu na Hadithi za Mtume zitafasirika kuwa ni pigo la aina fulani ya kuonesha hisia za kukerwa na kuonesha lawama ya kutoridhika na kitendo kilichotokea na haina maana kuwa umpige kwa kumuumiza na kumpa mateso ya mwili; lakini ikitokezea basi hubeba sura ya kupiga kwa mfano kwa (kutumia) mswaki ambao kikawaida huwa hautumiki kama ni kitu cha kupigia lakini ni ishara ya kuonesha kuwa umekasirika na pia kwa kutoa lawama.
Na pigo hili limehalalishwa na sharia kwa kuwekewa masharti kwa baadhi ya mazingira ya tamaduni ambazo mwanamke itabidi atendewe jambo hili na ili ahisi ujanadume wa mumewe. Na mazingira ya tamaduni hizo hazitambulikani na wamagharibi na wala hawajawahi kuziona, na Qur`ani Tukufu imekuja kwa watu wote na kwa nyakati na maeneo yote na kwa kila mtu mpaka siku ya mwisho, na ikakusanya mambo yake kwa kuzingatia mazingira ya tamaduni tafauti ambazo pindi Qur`ani Tukufu ingeliacha (kutozizungumzia) basi ingelionekana kuwa ina kasoro na ingelipelekea kupatikana kwa kuyumba kwa familia na kupelekea kuporomoka, hivyo kutajwa (pigo) imepelekea kuthibiti familia na kuwepo kwa masilahi.
Na katika dalili zenye kujulisha maana ya aya hii kuwa kuhalalishwa kupiga hakuhitajiki katika hali zote na kwa nyakati zote na mazingira yote ni kauli yake Mtume (Rehma na amani zimshukie) kuwa –imethibiti kutoka kwake kuwa kakataza kuwapiga wanawake akasema: “Msiwapige vijakazi wa Mwenyezi Mungu.”
Akaja Omar (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kwa Mtume (Rehma na amani zimshukie) akamshtakia ya kwamba wanawake wameasi kwa waume zao, hapo Mtume (Rehma na amani zimshukie) akatoa ruhusa ya kupiga kama ni ishara ya makemeo, na baadhi ya masahaba wakafahamu kimakosa kuona kuwa hiyo ndiyo ruhusa ya kupiga. Wake zao wakaenda kwa Mtume (Rehma na amani zimshukie) kumshtakia, hapo tena Mtume (Rehma na amani zimshukie) akawatolea ukali Maswahaba zake na kuwakasirikia kwa kuwaambia: “Katika nyumba ya watu wa Muhammad wamekuja wanawake wengi wanawashtakia waume zao, hivyo kwani hao si wake zenu.” Imepokewa na Abu Daudi katika kitabu chake.
Na hii ni dalili ya kuwa kupiga hakujahalalishwa katika hali zote, isipokuwa imekatazwa kabisa iwapo itakuwa ni kwa udhalilishaji au kumvunjia heshima au kumjeruhi na hiyo ndiyo maana ya kuzuia kwake Mtume (Rehma na amani zimshukie) wakati wa mwanzo kisha akaruhusu akiwa na malengo ya kukemea na kuonesha hasira tu na kitu cha kupigia kiwe ni mswaki na mfano wake katika vile vilivyopo katika mazingira ya tamaduni iliyozoelekana kwa Waarabu katika matukio kama haya, kisha (Mtume) akawakasirikia baadhi ya Maswahaba kwa kutumia nafasi hii vibaya na kuwanyima kheri wake zao, hapo katazo likajulisha kuwa kwa mara ya kwanza ilikuwa ni makatazo, kisha ikaruhusika (kwa mara ya pili) na kwa mara ya tatu ikawa ni kukebehi kwa maana kwamba uhalali wa kisheria juu ya jambo hili ukazingatiwa kama ni ada – desturi- ya kuonesha chukizo na kutoridhika, na kuwa utapatikana uharamu wa kupiga iwapo kutakuwa na majeruhi kwa mke, na jambo hili huenda likawa katika (baadhi ya) mazingira ambayo pindi likifanyika huwa halizingatiwi kuwa ni kumdhalilisha mke au kumtendea ubaya, pamoja na hivyo jambo hili huwa halifanywi na watu wenye heshima zao na walio wakarimu.
Twahir Ibn Ashur anasema katika tafsiri yake [At Tahri wa tanwir 5/41-42, chapa. Dar Sahnun Tunisia]: “Kwa mtazamo wangu naona kuwa habari zilizoelezwa zinazingatiwa kuwa ni halali kwa kuchunga ada za baadhi ya matabaka ya watu au baadhi ya makabila kwani watu wametofautiana juu ya swala hilo, kwani watu wa majangwani wao hawaoni kumpiga mke ni katika mambo ya uadui (mambo mabaya) wala wake zao hawaoni kuwa kupigwa ni katika kutendewa uadui… hivyo hapana kosa kwa kuruhusiwa watu ambao hawaoni tatizo (kwao si tatizo) iwapo watapigwa na waume zao kuwa ni makosa (madhara) au aibu au kuona kuwa wametendewa kitu kigeni katika familia na wala wake zao hawahisi chochote juu ya mualama kama huu.” Mwisho.
Na pia inafaa kwa hakimu kuwazuia waume kutekeleza jambo hili la kuwapiga wake zao iwapo watatumia vibaya amri ya kuhalilishwa kwake na watapewa adhabu pindi wakiitumia vibaya (sharia imemruhusu hakimu kuweka masharti kwa ajili ya masilahi); kwani baadhi ya waume hufanya kuwa ndio sababu ya kuwapiga wake zao au kutolea hasira zao na kufanya maangamizi yao na si kwa ajili ya kuleta masilahi, mwisho wake hutokezea yasiyotarajiwa ya kueneza roho za kiuadui katika maisha ya kifamilia.
Hivyo hakimu ana haki ya kuzuia kwa ajili ya kutela masilahi na kuondosha madhara au hata kama itatumika kama njia ya upatanisho kama inayotumika kwa wakati wetu huu na katika mazingira mengi, kwani watu wengi sasa wanatumia kupiga kama ni mojawapo ya namna za kuujeruhi mwili na kuuangamiza ikibidi, jambo ambalo ni haramu na wala hakuna tafauti yeyote kati ya wanazuoni juu ya jambo hili.
Tahir Bin Ashur anasema katika kitabu cha: [At tahrir wa tanwir (5/44): “Lakini pigo ni jambo la hatari na mipaka yake ni migumu kuielewa… isipokuwa Wanazuoni wengi wameweka masharti ya kuwepo kwa usalama wa kutopatikana madhara, na kufanyika kwa yule ambaye hata akifanya basi haitahesabika kuwa anadhalilisha au analeta madhara.
Hivyo tunasema: Inafaa kwa viongozi pindi wakielewa kuwa wapo waume ambao hawatekelezi adhabu hii kama sharia isemavyo na wala hawasimamii katika mipaka yake kwa kuwa wanapiga kwa mikono yao, basi wawaambie kuwa yeyote atakaempiga mkewe basi na yeye ataadhibiwa, kama alivyofanya na yeye atafanyiwa ili majanga ya kupigwa wake yasienee na hasahasa panapokuwa hapana uadilifu”. Mwisho.
Na hii ndio maana ambayo imeelezwa na kundi la Wasomi la kukataza kupiga, kama alivyosema mfasiri mahiri Atwaa bin Abi Rabbah – kama alivyopokea kutoka kwa kadhi Ibn Al araby Al maliki katika kitabu cha: Ahkamul kuran 1/536, chapa, dar Al kutub Al Elmiyah] aliposema: “Na wala hatampiga na kama atamuamrisha (jambo) au kumkataza na asitii (jambo) hilo, lakini (kitakiwacho) ni kumkasirikia tu.” Na wakaifasiri aya kwa maana ya kuonesha kutoridhika, na juu ya hili wanazuoni wengi wameunga mkono. Ibn Al fursi anasema: Na wamekana Hadithi iliyopokelewa yenye kujulisha kupiga, na amepokea kutoka kwa Twahir bin Ashuur katika tafsiri yake (5/43).
Hapana shaka ya kuwa pigo lenye kuumiza au kwa bakora au kuudhuru mwili, ambao huitwa: Ukatili ndani ya familia ni haramu kisharia. Na wanadamu wote inawalazimu kuipinga (tabia hii), na kutumia nguvu dhidi ya mke hakuhusishwi na Uislamu kwani vyanzo vya sheria ya kiislamu vinahimiza waislamu wawe na upendo na huruma katika maisha ya ndoa na wala haitakikani kwa namna yeyote ile kuwapiga wanawake na kuwadhulumu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na katika Ishara Zake ni kuwa Amewaumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao, naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika hayo zimo Ishara kwa watu wanaofikiri} [AR RUUM; 21] Na wasomi wa dini wanapinga kupigwa na kuwafnyia ukatili wanawake.
Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) ameweka wazi mahusiano ya mwanamke na mwanamme kuwa yapo kwa misingi ya upendo na huruma na hali hii inapingana na kupiga na kuumiza. Kwa hivyo Mtume (Rehma na amani zimshukie) anapinga sana na kwa nguvu zote jambo hili kwa kusema: “Hivi Mmjoja wenu anampiga mkewe kama apigavyo Mtumwa kisha anamuingilia mwisho wa siku?”. Imetolewa na Bukhari katika kitabu chake na [Al Baihaqi katika Sunan Kubra] kwa matamshi haya na kupitia Hadithi hii kuna jawabu kwa wanaodai kuwa Uislamu umehalalisha tendo la mume kumpiga mkewe.
Na asili katika sharia ni kuharamisha kero (maudhi) kwa namna yeyote ile, Mwenyezi Mungu anasema: {Na wale wanaowaudhi wanaume waaminio na wanawake waaminio pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba masingizio na dhambi iliyo dhahiri} [AL AHZAAB; 58] Na Mtume (Rehma na amani zimshuke amesema katika Hija ya kuaga: “Je nikuelezeni kwa mtu aliye muumini? Ni yule waliosalimika watu kutokana na mali zao na nafsi zao, na mwislamu ni yule waliosalimika watu kutokana na ulimi wake na mkono wake.” Imetolewa na Ahmad katika kitabu chake, na Ibn Hibban katika kitabu chake na wengineo.
Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) anasema: “Mgongo wa muumini umehifadhika isipokuwa kwa haki yake (isipokuwa ikibidi kupata hukumu)”, Imepokewa na Atwabarani katika kitabu cha: [Al muujamu kabiir] kutoka katika Hadithi ya Asmat bin Malik Al khutwami, na Imamu Bukhari kaifanyia mlango (sura) katika kitabu chake (Sahihi Bukhari): “Sura, mgongo wa muumini umehifadhika isipokuwa katika Haddi au kwa haki (kisasi)”.
Na Hafidh Bin Hajar amesema katika kitabu cha: [Fathu El Barin 12/85, chapa Dar Maarifa]: “(Umehifadhika) ikimaanisha, umelindwa na kupatwa na maumivu, na aliposema (isipokuwa kwa hukumu au haki) ikimaanisha kwamba, hapigwi na wala hadhalilishwi isipokuwa kama kuna hukumu au kupewa adabu.” Mwisho. (Na ijulikanavyo kuwa jambo hili lipo mikononi mwa sheria na kanuni na sio mikononi mwa watu.)
Na yaliyopo katika jamii ya kiislamu katika mambo hayo (ya kupiga) sababu yake ni waume kutofuata mafunzo ya dini yao njema, na wala haipasi kuunasibisha uislamu kwani hakuna mahusiano ya karibu wala ya mbali kati yake na matendo haya.
Na sheria zilizowekwa (za wanadamu) zitumikazo katika ulimwengu wa kisasa wa nchi za kiislamu zimetokana na sheria za kiislamu, zinaharamisha matumizi ya nguvu dhidi ya mwanamke (mke), na kufanya jambo hilo kuwa ni madhara yanayompasa mke kupewa haki yake kutokana na madhara ya kinafsi na kimwili na hupewa haki ya kudai talaka pamoja na kuchukua haki zake zote kamili bila ya kupunguzwa.
Imekuja katika kitabu cha: [(Wara wa kifamilia katika Uislamu] ambacho kimetolewa na Kamati ya Kimataifa ya Kiislamu kuhusu wanawake na watoto na kuandaliwa na Kamati ya Wanazuoni Wakuu katika ulimwengu wa Kiislamu akiwemo Mufti wa Misri (Uk 50): “Haifai – kwa namna yeyote ifikiayo ya tofauti kati ya wanandoa – kutumia nguvu zilizovuka mipaka iliyowekwa kisheria, na mwenye kupinga jambo hili basi atahusika kuwa ametenda kosa la jinai.” Mwisho.
Na imetajwa katika kifungu namba (6) katika sheria nambari 25 ya mwaka 1929 (kilichofanyiwa marekebisho kwa sheria nambari 100 ya mwaka 1985 AD.): “Iwapo mke amelalamika kupata madhara kutoka kwa mume ambayo hataweza kuendelea naye tena inafaa kwake (mke) kuomba kwa kadhi kutenganishwa (na mume wake.”
Na katika mifano ya kisharia ya madhara (yatokanayo na hali hii) ambayo inafaa kutoa talaka ni: Mume kumfanyia uadui mkewe kwa kumpiga na kumtusi.
Imetajwa katika mahakama za rufaa za Misri: “Hata kama kutii ni haki (wajibu) kwa mke juu ya mumewe lakini kwa sharti ambayo ni lazima mume awe mwaminifu kwa nafsi ya mke na mali yake, na hatamtii iwapo anamdhuru kwa makusudi; kwa kumshambulia kwa vitendo au maneno au kwa kuitawala mali ya mke kwa njia isiyo ya haki.” Mwisho. [rufaa nambari 116 ya mwaka 55, sheria za ndoa, kikao cha 24/6/1986 AD.]
Kwa mujibu wa yaliyotangulia: mume kumpiga mke wake na kumfanyia uadui na kumtisha pia na watoto ni katika mambo ambayo waislamu wote wamekubaliana kuyaharamisha, na wala hayana uhusiano na mafundisho ya uisllamu na sheria zake, jambo hilo ni makosa kisheria.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
